Wengi wanafikiria kuwa unene ni fahari, heshima, lakini huenda wanasahau au hawajui madhara mengi ambayo yamejificha nyuma yake
Imekuwa ikidhaniwa kuwa unene wa mwili ni kufanikiwa kiuchumi au kuukata, kumbe sivyo. Uchunguzi wa kitaalamu unaonyesha kuwa watu wanene wapo katika hatari ya kupata maradhi ya kiharusi, kisukari na ugonjwa wa moyo.
Matumizi ya baadhi ya vyakula na kutokujua chakula gani wale na kwa wakati gani bado ni tatizo.
Baadhi yao hula vyakula hivyo usiku, bila kujua athari kuwa vinazidisha unene na kuhatarisha maisha.
Wataalamu wanaeleza kuwa baadhi ya vyakula vikiliwa usiku husababisha athari kwa afya za watumiaji wake.
Athari kubwa zaidi ni kuongezeka uzito bila
mpangilio, kukosa usingizi na kulala kama mfu kutokana na tumbo kujaa,
vilevile kulala kwa usingizi wenye kukatikakatika, kujisaida haja ndogo
kila mara. Madaktari na wataalamu wengine wa afya wanashauri kwamba ili
kujiepusha na athari hizi ni vyema watu wanene wakatumia matunda,
mbogamboga au vyakula vingine ambavyo vina kalori na mafuta kidogo au
visiwe navyo kabisa.
Hivi ni baadhi ya vyakula ambavyo si vizuri kula wakati wa kwenda kulala kwa watu wanene na wenye uzito mkubwa.
Vyakula vilivyoandaliwa kwa mafuta mengi
Hii ni aina ya chakula ambacho hupaswi kula usiku
kwa sababu havikufanyi ujisikie uchovu na uvivu asubuhi ya siku
inayofuata, bali pia humpa msukosuko mtumiaji wa kwenda kujisaidia mara
kwa mara.
Pamoja na vyakula vya mafuta, ice cream ni tatizo
kwa kuwa ukila sukari unaongezeka uzito bila sababu, pia hujipa
msukosuko wakati wa kulala kwa kuwa baada ya muda huyeyuka na kuzaa
tatizo nyingine. Aina hii ya vyakula husababisha magonjwa ya kiharusi,
kisukari na ugonjwa wa moyo.
Kabohaidreti (wanga) kwa wingi au vyakula vyenye sukari kupitiliza
Kundi hili ndilo ambalo watu wengi hulichanganya
kwa kuamini kuwa tambi ‘supagheti’ ni chakula chepesi kuliwa usiku, kitu
ambacho si sahihi.
Tambi ni moja ya vyakula ambavyo havipaswi kuliwa usiku kwani
ina wanga mwingi ambao kutokana na kulala hakisagiki na kinaweza kuziba
mirija ya damu na kusababisha madhara kwa mtumiaji.
Kipande kidogo cha keki kinaweza kuwa kizuri kwa
mtumiaji, lakini akizidisha siyo nzuri kutokana na kuwa na sukari
nyingi. Vilevile mkate mweupe uepukwe una wanga mwingi.
Nyama nyekundu na vyakula vyenye protini nyingi
Kula nyama nyekundu usiku kunamfanya mhusika
asipate usingizi mzuri kwa kuwa tumbo linashindwa kusaga vyakula vigumu
uwapo usingizini.
Kama ni lazima kula nyama, basi ni vyema ikawa ni
nyama nyeupe kama vile kuku na samaki na kuepuka vyakula vyenye
protini. Ikishindikana, basi glasi ya maziwa ya moto inaweza kukidhi
haja bila kuwa na madhara.
Vyakula vyenye viungo vingi
Hupaswi kula vyakula vya aina hii kwa kuwa vina kemikali ambayo inaweza kukukosesha usingizi.
Kahawa
Kwa kawaida, kahawa ina kafeini ambayo inaweza
kusababisha usumbufu wakati wa kulala kwani hata dawa zenye kafeini
hapaswi kupewa mgonjwa mwenye matatizo ya kulala.
Vivyo hivyo, kwa asiyekuwa mgonjwa ina madhara pia
hapa hata soda ambazo zina kafeini, pia zinasababisha mtumiaji kukosa
usingizi wa kutosha, hivyo kushindwa kufanya mambo katika mpangilio
maalumu siku inayofuata.
Mtaalamu wa masuala ya chakula na lishe, Pazi
Mwinyimvua anasema kuwa kama ni lazima kunywa kahawa, basi iwe ni saa
tano au nne kabla ya kwenda kulala.
Pazi anasema kuwa kuna baadhi ya vitu vina madhara
kwa mtumiaji bila kujua kutokana na kuwa na mazoea ya kutumia kitu
hicho ambapo matokeo yake madhara yake huwa ni mhusika kupata tatizo la
kukosa usingizi.
Kula chakula kingi
Madhara ya kula chakula kingi ni mengi, mojawapo ni kukosa usingizi kutokana na kushiba kupita kiasi.
Athari za kufanya hivi ni pamoja na kuukosesha mwili uwezo wa kusaga chakula kwa kuwa utakuwa umeshiba sana na mwili umepumzika.
“Ukiwa katika hali hii hata usingizi unakuwa ni wa
shaka kwa kuwa unakuwa umeshiba sana, lakini hicho chakula hakifanyi
kazi ipasavyo na ndiyo maana ni rahisi kuongezeka uzito, hakimeng’enyeki
kwa urahisi,” anasema Pazi.
Vyakula vilivyokaangwa
Vyakula hivi husababisha kiu, hivyo humlazimu mtumiaji kunywa maji mengi na kumlazimisha kwenda msalani mara kwa mara.
Pazi anasema mwili unahitaji kupumzika kwa kulala kwa saa sita hadi nane ili ufanye kazi na mhusika akiamka aanze upya.
“Kkubwa hapa ni kupunguza kula vyakula ambavyo
vitahitaji maji au vyenye maji maji kuepuka kwenda msalani mara kwa mara
au kuamka
Pombe
Kunywa pombe saa chahe kabla ya kulala au kunywa
na kulala huku ukiwa nazo kichwani hata kama hujalewa siyo nzuri kiafya
kwa kuwa huufanya mwili kulala kama mzigo hivyo inakuwa siyo kupumzika
bali kulazimika kulala kwa ulevi.
Mtaalamu mmoja wa lishe anasema kuwa mwili
unahitaji kupumzika ukiwa huru na siyo kulazimishwa na kilevi, kwani
kupumzika ni pamoja na kufahamu sasa naenda kupumzika na mwili unauandaa
kwa ajili hiyo, lakini ukiwa umelewa hali kama hiyo haipo.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani (Mfumo wa
Chakula), Dk Raymond Mwenesano wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH)
anasema kuwa kwa kawaida mwili wa binadamu unapohitaji mapumziko au
unapofika muda wa kupumzika inabidi uwe huru kwa maana ya kuwa katika
hali ya kawaida, hususan sehemu za ndani kama tumbo.
Anasema kuwa kama utapumzika huku ukiwa na vitu vya ziada
ambavyo vitakuwa na usumbufu kwako kama kushiba, kulewa unakosa ile
dhana nzima ya kupumzika na matokeo yake ni kutimiza wajibu wa kulala na
si kulala kwa ajili ya kupata mapumziko.
Mariam Rashid, ambaye ni mnene kiwajihi anasema
kuwa tangu aanze kupunguza kula vyakula vyenye wanga wakati wa usiku
amepungua uzito kwani alikuwa ni lazima ale wali au chapati usiku na
kujikuta ana uzito mkubwa akashauriwa na daktari kupunguza uzito na kwa
kuanza alianza kupunguza kula na kushiba usiku ikiwemo kuacha vyakula
vyenye wanga.
“Nakula matunda na mboga mboga kabla ya kulala na
huu ni ushauri niliopewa na daktari wakati ambapo nilikuwa na uzito
mkubwa ilikuwa karibu kilo 70 wakati urefu wangu ni futi tano, ilikuwa
ni hatari na daktari alinikemea na kunitaka nipungue kwa kuwa nilikuwa
nimeshaanza kupata tatizo la miguu na kukosa usingizi,” anasema.
Mtaalamu wa masuala ya Saikolojia wa Chuo Kikuu
cha Dodoma, Modesta Kamongi amesema kuwa si tu unene unaohatarisha afya
ya mhusika, bali pia humfanya asijiamini.
Anasema ni vyema kila mmoja akawa na mwili wa
wastani kwani mara nyingi wamekuwa wakipata malalamiko kwa watu wanene
hujichukia na kutaka wapatiwe ushauri wa jinsi ya kukabiliana na wale
wanaowatania.
0 comments: